Jina : CHA.KI.TA
Makazi:  Nairobi, Kenya
Barua pepe:info@chakita.org
HISTORIA FUPI YA CHAKITA

Mnamo 1997 kamati ndogo ya kitaifa ya wahadhiri iliundwa mjini Eldoret kwenye warsha iliyoandaliwa na Idara ya Kiswahili Chuo Kikuu cha Moi ili kuchunguza uwezekano wa kuandaa Kongamano katika Chuo Kikuu cha Kenyatta mnamo 1998 na kushinikiza matumizi ya Kiswahili .

Kamati hiyo ikishirikiana na Idara ya Kiswahili ya Chuo cha Kenyatta, iliandaa Kongamano lenye mada ya Kiswahili Katika Karne ya 21. Ni katika Kongamano la Kenyatta ambapo dhana ya CHAKITA iliibuka. Kamati iliombwa ichukue wadhifa wa kusajilisha chama na kukiongoza huku ikishirikiana na chuo cha Maseno kuandaa Kongamano la 1999. Kamati ilifanya hivyo na ikaandaa Kongamano kuhusu Mustakabali wa Utafiti wa Kiswahili. Chama kiliandaa Kongamano mjini Mombasa Fort Jesus mnamo 2002 kuhusu Kiswahili kwa Mahitaji Maalum, na kilishirikiana na Chuo Kikuu cha Egerton kuandaa Kongamano kuhusu Lugha na Utandawazi.

Mnamo 2003 Chama kilishirikiana na Chuo Kikuu cha Nairobi kuandaa Kongamano kuhusu Kiswahili na Mikondo ya Fikra. Mwaka uliofuatia (2004) tulikutana katika Hoteli ya Silver Springs-Nairobi na kujadili kuhusu Fasihi Simulizi ya Kiswahili. Mwaka wa 2005 tulikutana Mombasa kuzungumzia juu ya Kiswahili na Elimu Nchini Kenya; 2006 tukatutana Hoteli ya Kunste-Nakuru kujadili Isimu Jamii ya Kiswahili na mwaka wa 2007 tukajumuika katika Chuo Kikuu cha Moi kujadili Kiswahili na Masuala Ibuka.

Mnamo 2008 tulikutana mjini Mombasa na tukajadili kuhusu Lugha, Utaifa na Utangamano. Mwaka wa 2009 tulishirikiana na Chuo Kikuu cha Nairobi kujadili kuhusu nafasi ya asasi mbalimbali katika ukuzaji wa Kiswahili na 2010 tulikutana katika Chuo Kikuu cha Pwani kujadili nafasi ya tafsiri.


Chama kimeweza kuchapisha vitabu vitano:


  1.Kiswahili: A Tool for Development – Chuo Kikuu cha Moi
  2.Kiswahili Katika Karne ya Ishirini Na Moja – CASAS, South Africa (2000)
  3.Utafiti wa Kiswahili – Chuo Kikuu cha Maseno / Chuo Kikuu cha Moi
  4.Fasihi Simulizi ya Kiswahili – Twaweza Communications (2006)
  5.Kiswahili na Elimu Nchini Kenya – Twaweza Communications (2007)

Vitabu vingine viko jikoni vikipikwa.
Chama kiliweza kutetea nafasi ya Kiswahili kwenye Kamati ya Wataalamu Kuhusu Katiba na sasa Kiswahili ni lugha ya taifa na rasmi nchini kwa mujibu wa Ibara 7 ya Katiba ya Kenya. Ushindi huu ni mchango mkubwa sana wa CHAKITA. Hatua itakayofuatia ni kuhakikisha kuwa nyaraka zote za taifa zinapatikana kwa Kiswahili. Serikali za Kaunti zitalazimika kutumia Kiswahili na Kiingereza katika shughuli zake.UONGOZI WA CHAKITA (2011)

Mwenyekiti : Prof. Kimani Njogu  
Naibu Mwenyekiti: Dkt.  Mwanakombo Noordin 
Katibu: Prof.: Clara Momanyi 
Naibu Katibu: Dkt. Issa Mwamzandi 
Mhazini:    Prof. Naomi Shitemi 
Naibu Mhazini: Dkt. Mwenda Mukuthuria 
      
Chama kina Kamati zifuatazo:
(a)Kamati ya Warsha za Shule
(b)Kamati ya Machapisho
(c)Semina na Makongamano
(d)Maendeleo
(e)Utaalamu/Akademia
(f)Ushirikiano

Kila Kamati ina mjumuishi na wanachama wake.