HISTORIA FUPI YA CHAMA CHA KISWAHILI CHA TAIFA – KENYA (CHAKITA)

Wazo la kubuniwa kwa Chama cha Kiswahili lilianzishwa mwaka wa 1997 katika Kongamano lililoandaliwa na Idara ya Kiswahili, Chuo Kikuu cha Moi.  Lengo la kongamano hilo lilikuwa ni kutathmini iwapo kulikuwa na uwezekano wa kuwa na kongamano ambalo lingewaleta pamoja wataalam wa Kiswahili nchini Kenya. Katika Kongamano hilo, kamati iliundwa ili ifanye kazi na idara ya Kiswahili, Chuo Kikuu cha Kenyatta ambacho kilikubaliwa kiwe mwenyeji wa Kongamano katika mwaka uliofuatia, 1998. Kupitia kwa juhudi za kamati na idara ya Kiswahili, Chuo Kikuu cha Kenyatta kongamano lenye kauli mbiu Kiswahili katika Karne ya 21 liliandaliwa.

Kamati andalizi iliyoteuliwa wakati huo ilipewa jukumu la kusajili wanachama kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Maseno ambacho kilikuwa kimependekezwa ili kuwa mwenyeji wa kongamano la mwaka uliofuata wa 1999. Maudhui ya kongamano hilo yalikuwa Mustakabali wa Utafiti wa Kiswahili. Kufikia wakati wa kongamano hilo, chama kilikuwa kimepiga hatua katika usajili wa wanachama wapya.

Azma ya chama hiki ilikwa kuanzisha jukwaa la wataalamu wa Kiswahili (wahadhiri na walimu wa Kiswahili) na wadau wengine ili kujenga jukwaa ambalo lingetumika kuboresha utaalamu na ubadilishanaji wa maarifa ya kitaaluma hasa kuhusiana na maendeleo ya Kiswahili na nafasi yake katika ujenzi wa taifa.

Uthabiti wa jukwaa hili ulikuwa katika imani kwamba Kiswahili hutekeleza majukumu muhimu  katika maisha ya watumiaji wake, si katika Afrika Mashariki pekee, bali pia ulimwenguni kote. Lugha ya Kiswahili pia ilikuwa imeonekana kuwa na uwezo wa kuteuliwa ili kuwa lugha ya taifa ya Kenya pamoja na Kiingereza, jukumu ambalo Kiswahili kilikuwa tayari kimetekeleza kwa mwongo mmoja tangu mwaka wa 2010 katiba mpya ilipozinduliwa. Kwa kuongezea, kulikuwa pia na mapatano miongoni mwa wanachama kwamba chama kikuze lugha hii ya Kiswahili ili kuinua hadhi yake inayostahili kama lugha ya kukuza maendeleo ya taifa.

Mnamo mwaka wa 2000, Chama kiliandaa Kongamano mjini Mombasa ambapo kauli mbiu ilikuwa Kiswahili kwa Mahitaji Maalum.  Utaratibu huu uliendelea hivyo na mwaka wa 2002, CHAKITA ikishirikiana na Chuo Kikuu cha Egerton ambapo idara ya Lugha  na Isimu iliandaa kongamano lililokuwa na kauli mbiu Lugha na Utandawazi na baaadye mwaka wa 2003 kongamano lingine likafuatia lenye kauli mbiu Kiswahili na Mikondo ya Fikra.  Makongamano mengine yaliyofuata ni kama yafuatayo: Nakuru (2006), Chuo Kikuu cha Moi (2007), Chuo Kikuu cha Nairobi (2009), Mombasa (2016), Chuo Kikuu cha Kibabii (2017), Chuo Kikuu cha Moi (2018), Chuo Kikuu cha Karatina (2019). Kongamano ambalo lingefanyika katika Chuo Kikuu cha Kabaraka mwaka wa 2020, halikufanyika kutokana na janga la COVID-19. Kongamano la 2021 litafanyika katika Kaunti ya Baringo (Kenya School of Government).

Kila mwaka Chama hutangaza rasmi makongamano. Aidha, huandaa kongamano moja ambapo wanachama hutaarifiwa kuhusu Wito wa Ikisiri kupitia kwa baruapepe na pia matangazo yanatanganzwa moja kwa moja kupitia tovuti rasmi ya chama, mitandao ya kijamii (kama ile whassap na nk). Malengo yatakuwa ni kuwafikia wataalamu wengi iwezekanavyo. Katika matangazo hayo, arifa muhimu zitatolewa kuhusu Kauli Mbiu, Mada, sehemu ya kongamano, ada ya ushiriki na makataa ya ikisiri na uandishi wa makala. Kadhalika, kutakuwepo arifa mbalimbali kuhusu makongamano ya awali ya Chama katika tovuti. Anwani maalumu ya mawasiliano itatolewa kwa ajili ya makongamano. Makongamano haya yanatarajiwa kulenga wapenzi na wataalamu wa Kiswahili. Pia, makataa hutolewa kwa wajumbe kutayarisha makala ambazo zitawasilishwa ili kuweza kushiriki kikamilifu katika makongamano hayo ya kila mwaka. Matukio muhimu yatatangazwa kupitia tovuti rasmi ya Chama. Chama kinakaribisha wajumbe kutoka Kenya na mataifa mengine ulimwenguni.

Yes, I need to attend this seminar! Save my seat today.

Chama cha Kiswahili cha Taifa
Facebook
Twitter
LinkedIn
JIUNGE NASI ILI KUPOKEA MACHAPISHO KWENYE BARUA PEPE

Jarida hili hutokea mara moja kwa mwaka (Novemba) na huchapisha makala ambazo hazijawahi kuchapishwa katika taaluma ya Lugha, Isimu na Fasihi ya Kiswahili na lugha nyingine za Kiafrika. Makala yasiyozingatia masharti yaliyowekwa na wahariri hayawezi kuchapishwa.