Makala haya yanashughulikia masuala kuhusu asasi ya ndoa za kisasa huku yakimulika uozo unaoshuhudiwa katika ndoa hizo, na wakati huo huo yatatoa suluhu kuhusiana na namna ya kukabiliana na uozo huo. Yatafanya hivyo kupitia uchanganuzi wa tamthilia teule, hususan tamthilia ya Mama Ee (Mwachofi, 1987) na tamthilia ya Nguzo Mama (Muhando, 1982). Fasihi ni fani hai ambayo inaendelea kutekeleza majukumu katika jamii ya kisasa inayobadilika. Fasihi hutoa mwonoulimwengu wa jamii na kutokana nayo, hali ya maisha ya kila siku huendelezwa. Kupitia kwa kazi za fasihi, jamii inayohusika huweza kutazamwa na kumulikwa katika nyanja mbalimbali. Wanajamii hueleza hali ya maisha, utamaduni, maoni, mitazamo, imani na mila zao kupitia fasihi - iwe ni andishi ama simulizi. Jamii ya kisasa inakumbwa na matatizo mengi, yakiwemo matatizo kuhusiana na asasi ya ndoa, magonjwa yasiyotibika, uraibu wa dawa za kulevya, ukosefu wa ajira kwa vijana, uabudu shetani, vita vya wenyewe kwa wenyewe miongoni mwa matatizo mengine. Ili kukabiliana na hali hizi ngumu, ni muhimu kuwa na nyenzo za mawasiliano zinazoweza kutumiwa kuwafahamisha na kuwatahadhalisha wanajamii kuhusiana na namna ya kukabiliana na matatizo wanayokumbana nayo maishani. Fasihi andishi ni miongoni mwa njia hizi kwani kupitia kwayo, ujumbe unaweza kuwasilishwa kuhusiana na matatizo yanayokumba jamii na maandishi hayo yakahifadhiwa kwa karne ili vizazi vya kesho vinufaike kupitia kwayo. Makala haya yanahoji dhima ya fasihi andishi ya Kiswahili kama nyenzo mwafaka ya kukabiliana na uozo katika asasi ya ndoa za kisasa. Nadhariatete inayojengwa na makala haya ni kwamba fasihi andishi hutumiwa na jamii inayobadilika kama nyenzo ya kupambana na masuala yanayotishia maendeleo endelevu katika jamii.