Itikadi za Kiuana katika Methali za Kinyankole

Methali huangazia masuala mbalimbali katika jamii. Methali aghalabu huchukuliwa kusheheni ukweli unaokubalika miongoni mwa wanajamii. Pamoja na mambo mengine, methali za Kinyankole hutekeleza dhima ya kuhifadhi historia na utamaduni. Isitoshe, falsafa na muonoulimwengu wa jamii ya Wanyankole pia husawiriwa katika methali zao. Kupitia semi hizo za kimapokeo, mila, desturi, amali na mawazo ya Wanyankole hurithishwa na kufahamika. Makala hii inachunguza itikadi za kiuana katika methali za Kinyankole. Itikadi za kiuana ni uthibitisho wa hadhi za kiuana zitokanazo na tathmini ya tofauti zake. Methali za Kinyankole zimechaguliwa kwa misingi kwamba ni utanzu wa fasihi simulizi unaosheheni mielekeo, mitazamo na falsafa za jamii. Tunachanganua jinsi itikadi za kiuana zinavyoendeleza mahusiano ya kiuana. Kwa kurejelea methali za Kinyankole, athiri za itikadi za kiuana kwa majukumu ya kiuana baina ya mwanamke na mwanamume zimejadiliwa. Kimsingi, Makala hii inabainisha jinsi itikadi za kiuana zinavyoendeleza mahusiano ya kiuana katika jamii mamboleo. Uchunguzi wenyewe umeegemezwa kwenye nadharia ya Itikadi, nadharia ya Uana na nadharia ya mabadiliko.
JIUNGE NASI ILI KUPOKEA MACHAPISHO KWENYE BARUA PEPE

Jarida hili hutokea mara moja kwa mwaka (Novemba) na huchapisha makala ambazo hazijawahi kuchapishwa katika taaluma ya Lugha, Isimu na Fasihi ya Kiswahili na lugha nyingine za Kiafrika. Makala yasiyozingatia masharti yaliyowekwa na wahariri hayawezi kuchapishwa.