Lugha na Uana: Sakata ya Nafsi

Lugha ni asasi aali ambayo wanadamu hutumia kuwasiliana mbali na kuwarahisishia kazi. Hata hivyo, asasi hii imetumiwa tangu azali kuzifinyanga nafsi za waja ili kubainisha tofauti baina ya wanaume na wanawake. Sakata hii ya nafsi imeendelea kudumaza nafsi ya kike na kudumisha ile ya kiume kutokana na jinsi lugha inavyotumiwa katika miktadha na hali mbalimbali. Suala la nafsi ni suala linalojikita katika mitazamo ya watu na jinsi wanavyopaswa kuishi kulingana na vitengo vyao vya kimaumbile ambavyo pia hutumiwa kuyaainisha majukumu yao. Kwa mfano, mtu anapozaliwa mwanamume, tayari jamii imeshamwandalia majukumu yake ambayo anahitaji kuyazingatia kulingana na jinsia yake. Majukumu haya huainishwa na jamii naye akapewa pia lugha anayopaswa kutumia anapowasiliana na wengine, wawe wanawake au wanaume. Nafsi yake hushehenezwa hisia zinazomtambulisha yeye ni nani katika jamii na majukumu anayopaswa kutekeleza. Makala haya yamedondoa mifano michache tu katika mawanda ya lugha ya kawaida ili kubainisha suala la nafsi, mifano ya maneno yanayoashiria magonjwa na jinsi yanavyoathiri nafsi ya kike pamoja na matumizi ya lugha katika fasihi ili kubainisha tofauti hizo za kiuana. Makala yanatoa mapendekezo kadha ya jinsi suala zima la uana katika lugha linavyoweza kushughulikiwa ili kufisha athari hasi dhidi ya nafsi ya kike.
JIUNGE NASI ILI KUPOKEA MACHAPISHO KWENYE BARUA PEPE

Jarida hili hutokea mara moja kwa mwaka (Novemba) na huchapisha makala ambazo hazijawahi kuchapishwa katika taaluma ya Lugha, Isimu na Fasihi ya Kiswahili na lugha nyingine za Kiafrika. Makala yasiyozingatia masharti yaliyowekwa na wahariri hayawezi kuchapishwa.