Makala haya yanaangazia methali za Kiswahili kama chombo cha ubainishaji na uhifadhi wa mazingira katika jamii. Methali ni semi muhimu na vijipumzi vya utamaduni katika mapokeo ya wenyeji wa Afrika Mashariki. Wanajamii wamekuwa wakizitumia mno katika mawasiliano ya ana kwa ana na kupitishia elimu. Baadhi ya viongozi wa serikali na wanaharakati wa uhifadhi wa mazingira wamekuwa wakilishughulikia suala lili kwa kutumia vitisho, nguvu na kauli zisizoeleweka kufasirika kwa urahisi. Kwa mwelekeo huo, umma mpana umekuwa ukihisi kushurutishwa kukidhi ‘mambo ya serikali’ au matilaba ya ‘wenye-nchi’. Aidha, wananchi wamekuwa wakilalamika kuhusu hewa chafu kutokana na taka mitaani, harufu mbaya inayokirihi, mioshi inayofuka viwandani, maji ya mito yaliyochafuliwa. Uharibifu wa mazingira ni zimwi linalolemaza maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika mataifa yanayoendelea. Hali inayotokana na vitendo vya makusudi vya binadamu kwa kufahamu au kutofahamu. Suala la uhamasishaji kuhusu uhifadhi wa mazingira linahitaji kuhusisha umma mpana kwa kauli teule za kitamaduni zinazoeleweka. Kupitia kwa methali za Kiswahili, wenyeji wa Afrika Mashariki wana ‘sauti moja’ inayoeleweka au kwa mafumbo. ‘Sauti’ hiyo hufasiriwa kwa kuzingatia vielelelezo vya vijiishara na vijiashiriwa vinavyotokana na utamaduni wa jamii. Zaidi ya kuwa ni kauli za ubainishaji, methali za Kiswahili ni zinaweza kuwa vito vya uelezaji na uelekezaji kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mazingira siyo tu katika ngazi za kijamii na kitaifa bali pia kimataifa. Azma ya makala haya ni kufafanua namna vipengele vya mazingira vinabainika katika methali hizo. Kadhalika, itapendekezwa jinsi zinavyoweza kutumiwa kujengea usemezano wa kimkakati katika uzinduaji na uhamasishaji wa umma mpana kuhusu uhifadhi wa mazingira katika mataifa ya Afrika Masahariki kwa sasa na mustakabali wake.