Wataalamu wengi wanakubaliana kwamba kuna uhusiano mkubwa kati ya tafsiri na utamaduni. Wananadharia wa nadharia ya tafsiri wa awali akiwemo Catford walichukulia tafsiri kama utaratibu unaohusisha hali ya kuchukua makala katika lugha moja na kuyabadilisha katika lugha nyingine kwa kuhakikisha kwamba maana katika lugha mbili zinazohusika zinalingana. Maelezo kama haya yalisisitiza kwamba tafsiri ni mchakato wa kiisimu. Katika miaka ya hivi karibuni tafsiri inachukuliwa kuwa na uhusiano na utamaduni wa lugha asilia na wa lugha pokezi. Maoni haya yanaongozwa na ukweli kwamba lugha sio tu njia ya mawasiliano bali hubeba utamaduni wa watu wanaoitumia kama lugha yao ya kwanza. Ni vigumu kutenganisha lugha na utamaduni. Kwa sababu hii shughuli yoyote ya tafsiri huhusisha lugha na utamaduni. Utamaduni ni jumla ya taratibu za maisha ya jamii. Taratibu hizi ni pamoja na mila na desturi, amali, itikadi, mielekeo, falsafa na utawala. Kwa hivyo, kwa njia hii sababu ya kufanya tafsiri ni kuendeleza mawasiliano kati ya jamii au nchi tofauti tofauti. Mtaalam wa tafsiri, Eugene Nida, amefafanua tafsiri kama mchakato unaohusisha kuzalisha makala asilia katika lugha pokezi kupitia visawe vya karibu katika kiwango cha maana na cha mtindo. Anasema kwamba ili lengo hili litimie lazima mtafsiri azingatie tofauti za kitamaduni kwa sababu tafsiri sio tu mchakato unaohusu umilisi wa lugha zinazohusika bali pia wa tamaduni zinazohusika. Msimamo wa makala haya ni kwamba tafsiri ni utaratibu unaohusu mwingiliano kati ya tamaduni mbili. Ni katika muktadha huu ambapo makala haya yanachunguza jinsi ambavyo utamaduni wa Waingereza ulivyokutanishwa na wa Waswahili kupitia tafsiri za msamiati wa serikali na bunge. Data itakayochanganuliwa inatokana na vyombo vya habari na tafsiri zinazofanyika katika bunge la Afrika. Lengo la uchanganuzi huu ni kubainisha mbinu zinazotumiwa katika kutafsiri msamiati wa serikali na bunge. Pia utaangazia iwapo tafsiri hizo zinahifadhi utamaduni asilia (foreignization) ama kuhifadhi utamaduni wa lugha pokezi (familiarization) au kuchanganya yote mawili. Makala yatachangia katika kutoa mapendekezo ya kuimarisha tafsiri za kitamaduni kutoka Kiingereza hadi Kiswahili.