Nadharia ya Metausasa katika Fasihi: Mifano kutoka Shujaaz

Fasihi imepitia mabadiliko kadha katika makuzi yake. Kuanzia fasihi simulizi (hadithi, semi, maigizo, ushairi simulizi, mazungumzo na ngomezi), ikaja fasihi andishi (riwaya, tamthilia, hadithi fupi na ushairi andishi) na kisha fasihi ya watoto na vijana inayohusisha michoro. Kufikia sasa fasihi ipo katika filamu na video. Mabadiliko haya bila shaka yanaambatana na mabadiliko ya namna jamii inavyoendelea kubadilika kijamii, kiuchumi, kiteknolojia na mifumo mingine ya jamii. Nadharia za uhakiki wa fasihi nazo zimeasisiwa kukidhi mahitaji haya ya ukuaji ya fasihi. Kuna zile nadharia asilia (urasimi, umuundo), nadharia nyambuaji (urasimi mpya, umuundo leo) na nadharia changamano (uhalisia, ujamaa n.k.). Nadharia hizi zinatumiwa na zinakidhi kikamilifu utunzi na uhakiki wa kazi za fasihi simulizi na fasihi andishi. Tukiangalia nadharia kama vile ya Usasa, baada yake kumetokea nadharia ya Usasaleo. Kisha baada ya Usasaleo kuna Metausasa. Lengo la sura hii ni kuonyesha namna ambavyo nadharia ya metausasa inavyojidhihirisha katika kazi ya fasihi. Ili kufanikisha haya tutahakiki namna mihimili yake inavyojitokeza katika kitabu cha vibonzo cha Shujaaz kama fasihi ya kimetausasa. Yaliyomo kitabuni humu yatafafanuliwa kwa kuongozwa na nadharia hii, maelezo na ithibati kutolewa kitabuni kwa njia ya maelezo. Matokeo yanadhihirisha namna fasihi za kimetausasa zilivyo kwa kutumia Shujaaz kama kifani. Maneno Muhimu: Metausasa, nadharia, fasihi, shujaaz
JIUNGE NASI ILI KUPOKEA MACHAPISHO KWENYE BARUA PEPE

Jarida hili hutokea mara moja kwa mwaka (Novemba) na huchapisha makala ambazo hazijawahi kuchapishwa katika taaluma ya Lugha, Isimu na Fasihi ya Kiswahili na lugha nyingine za Kiafrika. Makala yasiyozingatia masharti yaliyowekwa na wahariri hayawezi kuchapishwa.