Makala hii inaangaza ujenzi wa hejemonia ya Kizungu katika jamii za Kiafrika kupitia janibu ya Waacoli kama inavyodhihirika katika Wimbo wa Lawino. Ikizingatia nadharia ya baada ya ukoloni, inafafanua kuwa dhana hejemonia ina maana mbalimbali ambazo zinawiana. Lakini kwa jumla ni uwezo au mamlaka ambayo watu fulani wa tabaka la juu hasa viongozi hupata ama kwa kulaghai watawaliwa kwa njia fiche, kwa kuwalaghai kwa uwazi au kwa kutumia nguvu iwe ni za kisheria au kijeshi. Makala hii inabaini kuwa hejemonia hukuzwa na kuendelezwa katika jamii na watu wenye uwezo kama vile Ocol, mumewe Lawino. Katika Wimbo wa Lawino, ni bayana kuwa hejemonia haifai madhali inamfanya Mwafrika achukie mila na desturi zake huku akisifu na kuabudu tamaduni za kigeni. Lakini wakati watu wengi hawashughuliki kupambana na hejemonia hii, Lawino anafunga kibwebwe na kuikabili. Anaikabili kwa kupiga msasa juhudi za kudunisha utamaduni wa Mwafrika kupitia ujirembeshaji, chakula na afya ya watu, ngoma na mandhari zao na kadhalika kwa kukataa kutukanwa na kudhalilishwa. Makala hii basi inatoa sauti ya Lawino ambaye ni yahe katika kupinga ukoloni mamboleo katika jamii yake, na katika jamii za Kiafrika kwa jumla.
Maneno Muhimu: Hejemonia, Utamaduni, Baada ya ukoloni, Utambulisho na Elimu.