Ulimwengu wa sasa umeshuhudia athari chanya na hasi katika matumizi ya teknolojia. Kwa hakika, karibu kila eneo la
maisha ya binadamu katika ulimwengu wa sasa linashuhudia matumizi ya aina mbalimbali za teknolojia katika sekta
mbalimbali, iwe elimu, biashara na kilimo kwa lengo la kufikia malengo ya Maendeleo Endelevu. Haya ni malengo ya
matamanio ya ulimwengu yanayokusudiwa kuleta maendeleo ya kiuchumi, ujumuishwaji wa kijamii na uendelevu wa
mazingira. Mojawapo ya malengo ya maendeleo endelevu ni kutokomeza njaa, kuwa na uhakika wa chakula, lishe bora
na kukuza kilimo endelevu. Ili kufikia lengo hili, ni muhimu kilimo kiboreshwe, kikuzwe na kiwe endelevu ili ifikiapo
2030 tatizo la njaa liwe limekwisha. Vivyo hivyo, ni muhimu kuwashirikisha wakulima kupitia njia za mawasiliano
zinazopatikana kwa urahisi na zinazoeleweka. Lugha ya Kiswahili ina jukumu la kutekeleza mawasiliano miongoni
mwa wakulima kwa kuwa ni lugha inayowafikia watu wengi Afrika Mashariki. Katika enzi hii, nyenzo za kuwafikia
wakulima hazina budi kuhusisha TEKNOHAMA. Ni katika muktadha huu ambapo makala hii inalenga
kutathmini mitandao ya kijamii, hasusan YouTube na Facebook, kwa kubainisha aina ya ushauri unaotolewa kwa
wakulima na upokezi wake pamoja na changamoto zozote wanazokumbana nazo. Hatimaye, mapendekezo kuhusu
mikakati ya kukabiliana na changamoto hizo yametolewa.