Suala la uchi linajitokeza katika nyanja mbalimbali katika jamii zote ulimwenguni. Aidha, dini ndiyo moja kati ya asasi kongwe ambayo inajengwa zaidi na suala la uchi. Jijini Nairobi, mbele ya Mahakama ya Upeo, kuna sanamu ya mvulana ambaye yuko uchi na ameshika samaki, labda kuashiria uwazi na haki inayotarajiwa kupatikana katika asasi hii. Katika utendaji wa Embalu miongoni mwa Babukusu, uchi hujitokeza katika sura tatu kuu: uchi wa kutofunika sehemu nyeti za mwili wa bibadamu; uchi wa kuweka mambo ya siri wazi; na uchi katika kutotumia tafsida. Makala hii inalenga kubainisha kuwa uchi huu unaweza kutumiwa kama mbinu mbadala ya kuimarisha usalama katika jamii. Nadharia ya Jazanda itatumika katika kupasua istiari zinazotokana na sura hizo tatu za uchi ili kuzifasili. Nadharia ya Jazanda inashikilia kwamba, maumbo yanayoonekana wazi ni msingi kuntu wa kuelewa masuala ya kidhania na magumu zaidi katika jamii. Katika kufanya hivyo, makala imeangazia dhima ya uchi katika kutishia na kuimarisha usalama katika jamii kupitia kwa fasihi, hasa utendaji wa embalu miongoni mwa Babukusu. Baadhi ya maswali yanayoibuliwa na makala hii ni kama vile, Je, uchi ni ishara ya usafi na utakatifu wa moyo au kinyume chake? Ni ishara ya uasi na ulevi au kinyume chake?