Uhakiki Linganishi wa Kimofosintaksia katika Ngeli za Luganda na Kiswahili Sanifu

Luganda na Kiswahili sanifu hutumia mfumo mmoja wa uianishaji wa ngeli. Licha ya kuwa lugha hizi ni za nasaba moja, zinadhihirisha upekee katika uainishaji na matumizi ya ngeli kimofolojia na kisintaksia. Makala hii inachunguza uwiano na tofauti katika mifumo ya uainishaji wa ngeli za Luganda na Kiswahili sanifu kimofosintaksia. Ufafanuzi wa uhusiano na tofauti baina ya mifumo ya ngeli za lugha hizi na unanuiwa kuepusha mwingiliano kimatumizi. Hoja inayojengwa ni kwamba uwiano na tofauti katika matumizi ya mifumo ya ngeli kimofosintaksia baina ya lugha za kwanza na Kiswahili sanifu husababisha mwingiliano kimatumizi. Data ilitokana na uchanganuzi wa maandishi yaliyoandikwa kuhusu ngeli za Luganda na Kiswahili sanifu, mijadala na usaili wa walimu 30 wa Luganda na Kiswahili kutoka shule za upili 15 teule, wilayani Kampala, Uganda. Uchunguzi huu uliongozwa na mihimili ya sarufi bia na upatanifu ya nadharia ya Umilikifu na Uhusisho (Chomsky, 1981). Nadharia hii huonesha ubia wa lugha na hali ya vipashio fulani vya kisarufi kutawala vipashio vingine katika tungo. Matokeo yalidhihirisha kuwepo kwa uwiano na tofauti baina ya ngeli za Luganda na Kiswahili sanifu kimofolojia na Kisintaksia.Inatarajiwa kwamba makala hii itawafaidi walimu na wanafunzi kutambua dhima ya L1 katika ujifunzaji na matumizi ya L2.
JIUNGE NASI ILI KUPOKEA MACHAPISHO KWENYE BARUA PEPE

Jarida hili hutokea mara moja kwa mwaka (Novemba) na huchapisha makala ambazo hazijawahi kuchapishwa katika taaluma ya Lugha, Isimu na Fasihi ya Kiswahili na lugha nyingine za Kiafrika. Makala yasiyozingatia masharti yaliyowekwa na wahariri hayawezi kuchapishwa.