Unyambulishaji wa vitenzi ni mojawapo ya masuala yanayoshughulikiwa katika taaluma ya mofolojia katika lugha nyingi za Kiafrika. Makala hii inashughulikia unyambulishaji wa vitenzi katika Kigĩchũgũ, kwa kufafanua maana zinazowakilishwa na maumbo mbalimbali katika Kigĩchũgũ. Katika uainishaji wa Guthrie (1967), Kigĩchũgũ ni mojawapo ya lugha za Kiafrika ambayo hudhihirisha unyambulishaji. Nadharia ya Mofolojia Leksia (Kiparsky, 1982 na Katamba, 1993) na Kanuni ya Kioo (Baker, 1985) zimetumiwa kueleza maana za mofu nyambulishi katika vitenzi vya Kigĩchũgũ. Vitenzi vilivyotumiwa katika makala hii viliainishwa katika kauli sita za unyambulishaji na kujadili maana ambazo huwakilishwa na maumbo ambayo huundwa na mifanyiko ya unyambulishaji. Makala hii inachangia katika kuongeza maarifa ya kiutafiti kuhusu sarufi ya Kigĩchũgũ na kuhifadhi lugha ya Kigĩchũgũ katika maandishi kama mojawapo ya lugha za Kiafrika.
Maneno Muhimu: Unyambulishaji, Maana, Vitenzi, Kigĩchũgũ