Nafasi ya Kiswahili katika Utekelezaji wa Ajenda Nne Kuu: Uzalishaji Viwandani

Mnamo mwaka wa 2008, serikali ya Kenya ilizindua ruwaza ya 2030. Ruwaza hii inalenga kubadilisha taifa la Kenya kuwa taifa linaloinukia kiviwanda, lenye mapato ya wastani, na ambalo litawapokeza wananchi wake hali ya juu ya maisha kufikia mwaka wa 2030. Utekelezaji wa ruwaza ya 2030 umegawanywa katika vipindi vitano vya miaka mitano kila kimoja: 2008-2012, 2012-2017, 2017-2022, 2022-2027, na 2027-2030. Katika kipindi hiki cha tatu (2017-2022), serikali imechagua kushughulikia ajenda kuu nne ambazo zitaliwezesha taifa hili kufikia malengo yake ya kimaendeleo na hivyo basi kuafikia ruwaza ya 2030. Ajenda hizi kuu nne ni: uzalishaji au/na utengenezaji wa bidhaa viwandani, ujenzi wa nyumba zinazomudiwa na wananchi wa kadri, utoaji wa huduma za afya kwa wananchi wote, na uzalishaji wa chakula cha kutosha kulisha taifa. Ajenda hizi nne zinalenga kuafikia mipango ya katikati ya kipindi cha tatu cha ruwaza ya 2030 (Medium Term Plans 3 (MTP3)). Baadhi ya tafiti zilizofanywa zinadhihirisha kuwa wananchi wengi hawana uelewa kuhusu ajenda hizi nne (Ripoti ya Infotrack, Disemba 20, 2018). Kadhalika ajenda hizi zimekumbwa na vikwazo vya aina kadhaa, vikiwemo vya kifedha na vya kisheria. Makala hii inahoji jitihada za serikali ya Kenya ‘kuwauzia’ raia wake Ajenda Nne Kuu za kimaendeleo, hususan ile ya uzalishaji viwandani. Sababu zinazotinga uelewa wa ajenda hiyo miongoni mwa raia walio wengi zimeangaziwa na mchango unaoweza kutolewa na lugha ya Kiswahili katika kufanikisha utekelezaji wa ajenda hiyo kuelezwa. Maneno Muhimu: Ajenda nne kuu, uzalishaji viwandani, Uchumi, ruwaza ya 2030
JIUNGE NASI ILI KUPOKEA MACHAPISHO KWENYE BARUA PEPE

Jarida hili hutokea mara moja kwa mwaka (Novemba) na huchapisha makala ambazo hazijawahi kuchapishwa katika taaluma ya Lugha, Isimu na Fasihi ya Kiswahili na lugha nyingine za Kiafrika. Makala yasiyozingatia masharti yaliyowekwa na wahariri hayawezi kuchapishwa.